20 Mei 2020 - 12:56
Kabuga: Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari Rwanda afikishwa mbele ya Mwendesha Mashtaka

Felicien Kabuga mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ambaye alikuwa mafichoni kwa mudawa miaka 26 kabla ya kukamatwa wiki iliyopita nchini Ufransa, anatarajiwa kupandishwa Mahakamani jijini Paris Ufaransa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mfadhili huyo wa mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 jana alifikishwa mbele ya Mwendesha Mashitaka Mkuu katika mji mkuu wa Ufaransa Paris.

Mahakama ya Paris itaamua iwapo itamkabidhi Kabuga kwa Mahakama maalumu ya Kimataifa ambayo ilichukua nafasi ya ile iliyokuwa inashughulikia kesi za Kimbari nchini Rwanda iliyokuwa mjini Arusha nchini Tanzania au la.

Félicien Kabuga leo Jumatano alitarajiwa kusikilizwa na majaji, lakini kwa ombi la wakili wake, Emmanuel Altit, zoezi hilo limeahirishwa hadi Jumatano ijayo.

Majaji watakuwa na siku 15 za kuamua juu ya uhalali wa waranti ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama Maalumu ya Kimataifa ya IRMCT, mahakama ambayo ina majukumu ya kukamilisha kazi ya mahakama iliyokuwa inashughulikia kesi za mauaji ya kiimbari nchini Rwanda iliyokuwa mjini Arusha nchini Tanzania.

Kabuga mwenye umri wa miaka 84 alikuwa miongoni mwa watuhumiwa 11 waliokuwa wakisakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na hata kutangazwa dau la dola milioni tano kwa atakayetoa taarifa za kutiwa mbaroni mshukiwa huyo.

Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalijiri kwa muda wa siku 100 kuanzia Aprili 6 mwaka 1994 baada ya Rais Juvanal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote Wahutu, kupoteza maisha wakati ndege yao ilipotunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Shambulizi hilo lilipelekea wanajeshi wa Kihutu wa serikali na wanamgambo waitifaki waliokuwa na misimamo mikali kuanzisha mauaji ya kimbari kwa lengo la kuwaangamiza Watutsi waliokuwa wachache.